dc.description.abstract | Makala hii inaangazia mustakabali wa hadhira katika upokezi wa
ushairi huru wa Kiswahili. Mwanzoni mwa miaka 1970, ushairi huu
ulijitokeza kwa kasi na ulituhumiwa kwa kutozingatia arudhi za
kimapokeo. Watunzi wa awali wa ushairi huu walikuwa wataalamu
wa lugha na wahakiki wa fasihi; waliotoa maelezo muhimu kuhusu
dhana na sifa za ushairi wa Kiswahili. Kabla ya miaka 1960, ushairi
wa kimapokeo ulikuwa umesambaa na umezoewa katika jamii.
Kujitokeza kwa ushairi huru kulisababisha watunzi na hadhira
kugawanyika katika makundi: lile linalojinasibisha na arudhi, lile
lisilojinasibisha na arudhi, na lile linalojinasibisha kwa kiasi na
arudhi hizo. Katika miaka ya 1970, waliouendeleza zaidi ushairi huru
walikuwa ‘vijana’ waliobahatika kupata elimu ya juu katika taaluma
ya fasihi na walitarajia kuchangia katika ufafanuzi wa dhana na sifa
za ushairi wa Kiswahili kwa ujumla. Swali linalofafanuliwa katika
makala hii ni: kwa nini ushairi huru wa Kiswahili ni kivutio cha
wataalamu wa lugha na wahakiki wa fasihi? Nadharia ya Semiotiki
imetumika kufafanulia matini za lugha kama viishara na viashiria
vinavyohitaji kufasiriwa. Data ya uchanganuzi ilitokana na upitiaji
wa mashairi katika diwani teule za mashairi ya Kiswahili. Aidha, data
nyingine ilitokana na usaili na hojaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na
wataalamu wa lugha na fasihi. | en_US |